Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameitupia tena lawama kampuni ya Facebook akidai inakionea Chama Tawala cha Uganda (NRM) na wafuasi wake na kusema hajutii kuifungia Facebook Uganda.

Museveni amewataka wafuasi wake wasiwe na hofu kwani tangu Facebook ifungwe nchini humo hakuna kilichosimama na mambo yanakwenda huku akisisitiza kuwa Facebook sio Mungu.

“Tangu Facebook iondoke (Uganda), mliwahi kusikia kuna uhaba wa sukari mjini? hamna nguo?, Facebook itaongea lakini tutasonga, wao sio Mungu,” amesema Museveni.

“Katika baadhi ya nchi hawaruhusu Facebook, je Facebook wanafanya kazi China? tuachane na hayo, nimesikia Mungu yupo kila mahali na anafahamu kila kitu, sijawahi kusikia kwamba Facebook iko katika kitengo hicho (cha kuwa kila mahali na kufahamu kila kitu)” amesisitiza Museveni.

Facebook ilizifunga akaunti za NRM wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Januari 2021, wakizituhumu kuhusika na vitendo visivyofaa.

Mtandao wa Facebook haupatikani bila VPN hadi sasa Uganda tangu ulipopigwa marufuku na Museveni wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Uganda ulifanyika Januari 14, 2021.

Othman Masoud aapa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar
Hitimana: Wachezaji wangu wana matatizo