Mwenyekiti wa Mbeya City  FC, Mussa Mapunda amelipongeza shirikisho la  soka Tanzania  TFF kwa hatua yake ya kuipoka  pointi 3 timu ya Azam Fc na  kuziweka kwa timu yake  kufutia  makosa yaliyofanywa na timu hiyo ya  Chamazi Complex  kumchezesha mchezaji Erasto Nyoni aliyekuwa na zuio la kadi tatu za njano.

Muda mfupi uliopita Mapunda ameimbia mbeyacityfc.com kwamba kwa kosa  hilo City ilistahili kupata ushindi huo wa bao 3 na pointi 3 kama ambavyo kanuni za ligi  zinavyoelekeza na kutoa  angalizo kwa vilabu vyote vinavyoshiriki ligi kuu Tanzania  bara kuongeza umakini katika  kutunza  kumbukumbu  za adhabu  au makosa mbalimbali kwa wachezaji wake.

“Kwenye hili nalipongeza shirikisho, hakika wametenda haki, na ninawaomba  waendelee kusimama kwenye misingi ya haki, ni haki yetu kupata pointi 3 baada ya Azam fc kuchezesha mchezaji mwenye adhabu ya kadi 3 ambaye ni wazi hakustahili kucheza mchezo ule, hata sisi tumekutana na hali hii katika nyakati tofauti lakini hatukuwahi kuthubutu kumchezesha mchezaji  mwenye adhabu  hata kama alikuwa ni muhimu kikosini” alisema.

DSC_00225 Mussa Mapunda Mwenyekiti wa Mbeya City

Akiendelea zaidi Mwenyekiti Mapunda alisisitiza vilabu kuwa makini na matukio ya aina hii  huku pia  akiikumbusha TFF kuendele kuchukua hatua kama hizi.

Katika hatua nyingine  Mapunda amesema kuwa  bado anaamini TFF itaitendea haki City kwa kuchukua hatua kama hizi kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union uliovunjika  dakika mwisho za kipindi cha pili baada ya kutokea kwa vurugu kubwa  uwanjani zilizosababishwa  na mashabiki wa timu hiyo ya Tanga.

“Naamini TFF watatutendea haki kwenye hili pia,mchezo ule ulikuwa na matukio mengi ya ajabu ambayo yalimfanya mwamuzi kushindwa kumaliza mchezo, risasi za moto zilipigwa  uwanjani, , sisi bado tunasubiri pointi tatu zingine kutoka kwenye mchezo ule, kwa sababu mnyonge mnyongeni  haki yake mpeni”, alimaliza.

Sauti: Wabunge wanawake Chadema wasusa baada ya kuambiwa wamepata Viti Maalum kwa ngono
Azam FC Yaanza Safari ya Kuelekea Mkoani Shinyanga