Mwalimu wa wa kike wa shule ya msingi ya Unga Limited mkoani Arusha alitekwa na watu wasiojulikana waliotishia kumpiga risasi endapo ataendelea kufuatilia sakata lake la kuvuliwa madaraka ya uratibu elimu kata ya Ngarenaro.

Mwalimu huyo aliyetajwa kwa jina la Batuli Isaya alisema kuwa alitekwa Oktoba 3 mwaka huu kwa kunyooshewa bastola na mtu asiyemfahamu alipokuwa anatoka dukani kununua vocha. Alisema mtu huyo alimuelekeza kuingia kwenye gari jekundu lililokuwa karibu naye.

Mwalimu huyo alisema kuwa baada ya kuingia kwenye gari hilo aliwakuta vijana wawili waliokuwa wamevalia kofia na kuficha sura ambao walimuonya kuwa asijaribu kufuatilia suala lake la kuvuliwa cheo.

Alisema kuwa baada ya gari hilo kufika katika eneo la Majengo, alipiga kioo kwa nguvu na kukivunja huku akipiga kelele lakini alizibwa mdomo na pua kwa kitambaa na hajui kilichoendelea baada ya hapo hadi alipojikuta amelazwa katika hospitali ya Mount Meru.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alithibitisha kupokea taarifa hizo na kueleza kuwa wameanza kufanya uchunguzi lakini hawajamkamata mtu yoyote kutokana na tukio hilo. Mwalimu huyo aliokotwa hajitambui katika eneo la Majengo.

Mume wa mwalimu huyo, Deus Mihambo alisema kuwa madaktari wamemchunguza na kubaini kuwa hakubakwa. Aliongeza kuwa wanaendelea kufanya utaratibu wa matibabu ikiwa ni pamoja na kumpima sumu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Athumani Kihamia aliliambia gazeti la Mwananchi kuwa kuvuliwa madaraka au kupewa madaraka ni jambo la kawaida linalofanywa na mwajiri.

Majaliwa apokea msaada wa sh. mil. 27.62, Tetemeko Kagera
Hekima za Nyerere zilivyomstaajabisha Gaddafi akazika uadui na kuwa Rafiki Mkubwa