Askari wa Makao Makuu ya Jeshi Polisi jijini Dar es Salaam jana walimkamata na kumshikilia mwandishi wa Dar24, Chis Kika kwa kuandika habari kuhusu Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Andrea Tsere KUKANUSHA taarifa zilizoandikwa mitandaoni kuwa alilazwa chooni katika mazingira ya kutatanisha.

Kika amesafirishwa chini ya ulinzi wa polisi mapema leo kwenda Wilayani Ludewa kujibu tuhuma zinazomkabili.

Mwandishi huyo wa Dar24 aliandika habari yenye kichwa cha habari ‘DC akanusha kulala chooni na familia yake, asema hatishiki’. Katika habari hiyo mwandishi alimmnukuu Mkuu huyo wa wilaya ya Ludewa kuwa ‘ALIKANUSHA’ taarifa za zilizokuwa zimesambazwa mtandaoni na watu wasiomtakia mema.

Wakielezea mazingira ya kukamatwa na kushikiliwa kwa mwandishi huyo kutokana na kuandika habari hiyo ya kukanusha uzushi, uongozi wa Dar24 umesema kuwa askari ambao awali walitumia utambulisho bandia kuwa wanatokea Benki ya CRDB, walimchukua Kika na wenzake wawili na kuwapeleka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi ili kuhojiwa na wataalamu wa makosa ya kimtandao kwa madai kuwa habari hiyo inahusika na uvunjifu wa sheria ya Makosa ya kimtadao.

Baada ya mahojiano ya awali, Polisi waliwaachia wenzake na kuendelea kumhoji Kika kwa zaidi ya saa tano ambapo alitoa ushirikiano wa kutosha. Kika alikiri kuwa ndiye aliyeandika habari hiyo ya kumkunukuu Mkuu wa Wilaya akikanusha taarifa zilizotolewa awali na vyombo vingine vya habari, siyo Dar24. Na kwamba alifanya hivyo kwa nia njema ya kusaidia kufikisha ujumbe wa Mkuu huyo wa wilaya dhidi ya wanaomzushia.

Kika alionesha kushangazwa na madai kuwa taarifa hiyo inamkashfu mkuu huyo wa wilaya na badala yake alieleza kuwa ilikuwa ikisaidia kufuta habari ya uzushi na kusisitiza kuwa alinukuu alichokisema Mkuu huyo wa Wilaya ya Ludewa kwa nia njema, hivyo alipaswa kupongezwa na sio kukamatwa.

“Nilitegemea kuwa Mheshimiwa DC angetushukuru Dar24 kuwa tumemsaidia kufikisha kwa umma taarifa inayomsafisha dhidi ya kile alichokiita njama ya kumkwamisha badala ya kuagiza nikamatwe na nisafirishwe chini ya ulinzi kwenda Ludewa kujibu mashtaka ya kuwa nimemkashifu. Yeye alikanusha na vyanzo vingi vilimnukuu alitegemea tuandike nini?” Kika alihoji.

“Mimi sielewi, mnasema DC wa Ludewa anadai nimemkashfu kwa kuwa nimeandika kuwa alikanusha kuwa yeye na familia yake walilazwa chooni? Kwahiyo anamaanisha hakukanusha?” Kika aliongeza.

Baada ya kusikiliza na kuandika maelezo ya Kika, askari Polisi wa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi walisema wao wanatekeleza maagizo ya Mkuu wa Wilaya ya Ludewa na hivyo hawakuwa na uwezo wa kushughulikia jambo lolote ikiwemo kumpatia dhamana mtuhumiwa. Hivyo, waliendelea kumshikilia wakisubiri kumsafirisha chini ya ulinzi kwenda Ludewa mapema leo kwa hatua zaidi.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, askari polisi aliyejieleza kuwa ametumwa kutoka Ludewa kutekeleza ukamataji wa Kika, alikataa kuzungumza na Mwanasheria wa Dar24 kuhusu hatua zinazochukuliwa kumsafirisha mteja wake ambaye alikuwa anaumwa, ikiwa ni pamoja na kufahamu namna atavyoweza kutumia dawa alizokuwa akiendelea kutumia.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha uhakika, Kika akiwa chini ya ulinzi wa askari polisi huyo kutoka Ludewa tayari yuko safarini kwenda Ludewa kujibu tuhuma zinazomkabili, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni utekelezaji wa sheria za makosa ya mtandao.

 

Josep Maria Bartomeu: Messi Na Suarez Watasaini Mikataba Mipya
Aliyetobolewa macho na ‘Scorpion’ asimulia mkasa mahakamani