Mwenyekiti wa CHADEMA, Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Erasmus Libaba amekamatwa na kuhojiwa kwa kosa la kupandisha bendera ya chama hicho katika barabara ambayo viongozi wa serikali wanapita wakiwa kwenye msafara.
Tukio hilo lilitokea Jumanne iliyopita ambapo Libaba alikamatwa na polisi kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa kisha kuwekwa ndani hadi alipoachiwa siku iliyofuatia yaani Jumatano.
Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu mkasa huo, Libaba amesema wamekuwa na utaratibu wa kupandisha bendera za Chadema asubuhi na kuzishusha jioni, “kwani tukiziacha, watu wasiojulikana wanazishusha usiku.”
RC Chalamila atangaza bakora kwa wasioa na kuolewa Mbeya
“Hawashushi tu bali wanavunja na mashina yetu yanayotumika kushusha bendera,” alisema Libaba.
Mwenyekiti huyo alisema, “siku moja kabla ya viongozi wa serikali kuja Ruangwa, vijana wetu walizuiwa kupandisha bendera lakini mimi nikawaambia kwa nini watuzuie wakati Katiba na sheria za nchi zinaturuhusu, Sasa…Jumanne ilikuwa kama saa 4 asubuhi, tukiwa kijiweni kwetu Mitope, alikuja mkuu wa wilaya akiwa na polisi na watu wengine, vijana walipoona vile walikimbia nikabaki mimi.”
Mwenyekiti huyo alisema, “nilikaa kituoni hadi jana (juzi) saa saba hivi waliponihoji kwa nini nilipandisha bendera za Chadema katika barabara ambayo viongozi wa Serikali wanapita, mimi nikawaambia sioni kosa lolote.”
“Sasa nikajiuliza kwani kuna kosa kupandisha bendera. Waliniachia na kunitaka kuripoti tena kituoni Jumatatu. Lakini nimweleze mkuu wa wilaya afuate katiba na sheria za nchi, Chadema ni chama kimesajiliwa, kinaruhusiwa kupandisha bendera zake,” alisema.
Hata hivyo, alipoulizwa kwa nini aliamuru akamatwe, Mkuu wa Wilaya, Mgandilwa alisema “suala hilo ni la kimahakama.”
Mwananchi lilipotaka kujua zaidi hadi anatoa amri kulikuwa na viashiria gani, mkuu huyo wa wilaya alisema suala hilo linaendelea kushughulikiwa.
Akizungumzia Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema kitendo hicho kinapaswa kukemewa.
Dk Mashinji alisema wanasubiri Libaba afikishwe mahakamani na “kama watamshitaki kwa kupandisha bendera za Chadema itakuwa kesi ya kuvutia na nitapenda mawakili wangu wawepo.”