Askari na Maafisa wa Jeshi la Polisi Nchini wameaswa kutotumia madaraka yao vibaya kwa kuwabambikizia wananchi kesi kwani kufanya hivyo ni kushindwa kusimamia dhamira njema ya Rais ya kuwapatia wananchi wanyonge haki zao stahiki.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba wakati akifungua kikao cha kazi cha Siku tatu cha mwaka 2017 kwa maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa LAPF Mjini Dodoma.
Amesema kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya kuwabambikizia kesi, Kuwabadilishia watu kesi zao za msingi kwa sababu ya kushindwa kutoa rushwa hivyo kikao hicho kinapaswa kuwa na maamuzi na maadhimio yenye dira na taswira njema kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Aidha, akizungumzia Vita dhidi ya Dawa za Kulevya, Nchemba amesema kuwa Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kukamata na kuziteketeza Dawa za kulevya zilizopo mashambani ambapo ametilia msisitizo zaidi kwa Askari na Maafisa wa Jeshi la Polisi kuendelea kupambana ili kukamata Dawa za kulevya zilizopo katika viwanda.
Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Polisi Nchini, Ernest Mangu amesema kuwa kikao hicho cha kazi kwa Maafisa wa Jeshi la Polisi kina dhamira kubwa ya kufanya Tathmini ya utendaji wa mwaka 2016 na kuandaa mikakati mizuri ya mwaka 2017 na kupata fursa ya kubadilika kiutendaji kwa kuzingatia dhamira ya Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Lugimbana amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa linayofanya ambapo pia amesema kuwa mpango wa Mkoa katika kupambana na migogoro ya ardhi kwa kuanzisha kamati maalumu ya wataalamu wa sheria kutoka chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) Kupitia na kushauri ili kuweza kumaliza haraka migogoro hiyo.