Rais Uhuru Kenyatta ameitisha mkutano wa kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) leo Jumatatu Juni 20, kujadili amani na usalama katika taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kutokana na taarifa yaa serikali ya Kenya, mkutano huo unakuja wakati mapigano makali yanafufua chuki za miongo kadhaa kati ya Kinshasa na Kigali, huku DRC ikiilaumu nchi jirani ya Rwanda kwa kufadhili kundi la waasi la M23.
Rwanda imepinga mara kadhaa made hayo huku nchi zote mbili zikilaumiana kwa kufanya mashambulizi ya kuvuka mpaka.
Rais Uhuru ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Juni 15, alitoa wito wa kupelekwa kwa Kikosi cha Kudumu cha Afrika Mashariki ili kukomesha ghasia katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo.
Hata hivyo, DRC inapinga Rwanda kuwa sehemu ya jeshi lililopendekezwa la kikanda na imesitisha uhusiano wa pande mbili na Kigali.
Rais Felix Tshisekedi katika taarifa yake aliishutumu Rwanda kwa kutaka kuikalia kimabavu nchi yake ili kutumia madini yake na kuitaka Uingereza kuishinikiza Kigali kukomesha uchokozi wake.
Katika taarifa kuhusu mkutano huo Kenyatta alisema, “Watu mashariki mwa DRC wameteseka kwa muda mrefu na wanaendelea kulipa gharama kubwa kupita kiasi kwa kupoteza maisha, mali na amani inayotoweka.”
Rais Kenyatta alisema jeshi la kikanda litafanya kazi pamoja na mamlaka za mkoa na kwa uratibu wa karibu na MONUSCO kuwapokonya silaha mtu yeyote anayebeba silaha kinyume cha sheria.
Kenya ndio mwenyeji wa mazungumzo ya moja kwa moja ya amani kati ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na makundi tofauti vya waasi.