Baada ya kumalizana na Singida Big Stars kwa kupata alama tatu muhimu jana Alhamis (Mei 04), Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi ametoa kauli ya kibabe na kuthibitisha kuwa tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Nusu Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini.

Young Africans itaanzia nyumbani Mei 10 katika Uwanja Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kwa kuikaribisha Marumo ambayo itafunga Safari kutoka nchini kwao Afrika Kusini, ambako utacheza mchezo wa Mkondo wa Pili Mei 17.

Kocha Nabi amesema tayari amewaona wapinzani wao hao na kuanza kuandaa mpango wa kumaliza mchezo wa Mkondo wa Kwanza, ambao amekiri utakuwa na changamoto kubwa ya upinzani.

Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema hana budi kujipanga kutokana na mazuri na udhaifu wa wapinzani wao aliouona, licha ya siku kadhaa kusalia kabla ya mpambano huo kupigwa jijini Dar es salaam juma lijalo.

“Tunafahamu kuna siku chache zimesalia kuelekea mchezo wetu wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ni mchezo ambao tunaanzia nyumbani, hivyo ni lazima tujitahidi kupata matokeo hapa na kumaliza hesabu kabla ya mchezo wa Mkondo wa Pili.”

“Tayari nimepata nafasi ya kuona ubora na mapungufu yao, ndani ya siku zilizosalia tutayafanyia kazi mazoezi na tunaamini tutafanya vizuri.” Amesema Nabi

Young Africans inaelekea katika mchezo huo wa Kimataifa, huku ikiwa na deni la alama tatu ili kutangaza Ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo, kufuatia ushindi wa 2-0 waliouvuna jana Alhamis (Mei 04) dhidi ya Singida Big Stars, iliyokuwa nyumbani Uwanja wa CCM Liti.

Historia kuandikwa soka la Saudi Arabia
Ukabila, Udini watajwa mapigano yanayoendelea Sudan