Kocha Mkuu wa Yanga, Nassredine Nabi amesema anaendelea kukisuka kikosi chake kiwe bora zaidi na tishio, lakini ataendelea kuwa mkali kuhusu suala la nidhamu ndani na nje ya uwanja, kwani timu hiyo ni kubwa zaidi ya mchezaji.
“Tangu nimekuja hapa nimekuwa nikifuatilia mienendo ya wachezaji wangu, nataka kujenga kikosi imara kitakachoogopeka Afrika, nitafanikiwa katika hilo iwapo suala la nidhamu litakuwa vizuri.”
“Nami nitasimamia hilo bila kuangalia kiwango cha mtu, anayeweza kufuata matakwa ya klabu tutaendelea kuwa naye, atakaeshindwa kuendana na kasi yetu milango iko wazi, malengo yetu ni kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa hapo mwakani,” amesema.
Nabi alisema kikosi chake kinahitaji kufanyiwa marekebisho ili kuendana na ukubwa wa timu kwa kufanya usajili wa wachezaji wenye uwezo mkubwa, hivyo anatarajia kufanya usajili katika baadhi ya maeneo ili kufanya maboresho.