Wakati Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC wakisafiri kuelekea Jijini Mwanza tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting utakaochezwa keshokutwa alhamis (Juni 03) katika Uwanja wa CCM Kirumba, Kocha Mkuu wa timu hiyo Didier Gomes amefichua siri nzito, kuhusu kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrson.

Gomes ambaye amekua akimtumia Morrison kama silaha ya kuwaangamiza wapinzani katika michezo ya Ligi Kuu, amesema kiungo huyo amekua silaha nzito ambayo hupenda kuitumia pale inapomlazimu.

Amesema mchezaji huyo ambaye alizua Songombingo wakati akijiunga na Simba SC akitokea Young Africans mwanzoni mwa msimu huu, amekua na utofauti mkubwa kikosini kwake, hali  ambayo anaichukulia kama hazina kubwa ya mafanikio.

“Morrison ni mchezaji spesho. Ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana. Ni hatari sana anapoenda mbele kushambulia,” amesema Gomes.

Lakini akatoa siri ya namna anavyomtumia mshambuliaji huyo katika michezo muhimu ambayo wanahitaji kucheza kwa tahadhari zaidi, ili kutimiza lengo la kuondoka na alama tatu muhimu.

“Katika michezo inazohitaji kuwa na mizani sawa katika kujilinda, nachezesha wachezaji wanaoendana zaidi na staili hiyo, kwa sababu Morrison hayuko vyema sana timu inaposhambuliwa. Lakini tunapohitaji kwenda kutafuta mabao, Morrison ni mtu sahihi kabisa kwa sabau ana uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi,” alisema kocha huyo Mfaransa.”

Morrison aliifungia bao la tatu Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC uliochezwa mkoani Lindi mwishoni mwa juma lililopita, akichukua nafasi ya Mzamiru Yassin katika kipindi cha pili.

Dakka 45 za mchezo huo zilishuhudia Simba SC wakienda mapumziko wakiwa nyuma kwa bao moja, lakini waliporejea kipindi cha pili walipata mabao ya ushindi kupitia kwa Criss Mugalu, John Bocco na Morrison.

Simba SC inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikifikisha alama 64, ikifuatiwa na Young Africans yenye alama 61, huku Azam FC ikiwa katika nafasi ya tatu kwa kumiliki alama 60.

Ujenzi wa mwendokasi hauridhishi - Rais Samia
Rais Samia asisitiza watanzania kujikinga na corona