Klabu ya Polisi Tanzania imewatumia salamu  Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, kuelekea mchezo utakaozikutanisha pande hizo mbili katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza baadae mwezi huu.

Simba SC kwa sasa ipo Jijini Mwanza ikitarajia kucheza dhidi ya Ruvu Shooting keshokutwa Alkhamis (Juni 03), kwenye uwanja wa CCM Kirumba.

Afisa Habari wa Polisi Tanzania FC, Hassan Juma amesema mikakati yao ni kushinda michezo yote minne ya ligi iliyosalia, ili kutimiza azma ya kumaliza nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Amesema kutoka na mikakati hiyo, hawana budi kujiandaa ili kufanikisha lengo la kuwabamiza Simba SC, kama walivyofanya Jijini Tanga ambapo waliacha kilio kwa Wagosi wa Kaya ‘Coastal Union’ mwezi uliopita.

“Askari wa mwamvuli wapo na morali ya kwenda kuhakikisha malengo ya timu msimu huu yanaweza kufikiwa kwa kukusanya alama 12 kwenye michezo minne iliyosalia kuanzia ule wa Juni 19 dhidi ya Simba,” alisema Juma.

Amesema Simba ni timu kubwa na wanaiheshimu imetoka kucheza mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini watapambana kuhakikisha wanachukua alama tatu kwao na kuwataka kwenda wakiwa wamejipanga vilivyo.

Simba SC inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikifikisha alama 64, ikifuatiwa na Young Africans yenye alama 61, huku Azam FC ikiwa katika nafasi ya tatu kwa kumiliki alama 60.

Waziri Ummy atangaza waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano, vyuo 2021
Ujenzi wa mwendokasi hauridhishi - Rais Samia