Nahodha wa klabu bingwa Tanzania bara Dar es salaam Young Africans, Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’ amejibu tambo za Nahodha wa Azam FC, John Raphael Bocco ‘Adebayor’.

Bocco alisema kwamba wataifunga Yanga SC Jumamosi Uwanja wa Taifa Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Lakini Cannavaro amemjibu; “Hizo ni ndito za mchana, sisi ndiyo tutawafunga wao,”amesema Cannavaro ambaye pia ni Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

“Sisi kwa kweli timu yetu imezidi kuimarika msimu huu na ninaamini Azam FC tutawafunga Jumamosi, wakibahatika sana watapata sare, na hiyo sare waitolee jasho haswa,”amesema.

Bocco alisema; “Tunawajua Yanga, ni timu nzuri kweli. Lakini sisi tunajua namna ya kuwafunga. Na tutawafunga tu,”.

Mechi mbili za awali msimu huu kuzikutanisha Yanga na Azam FC kila timu ilishinda moja, tena kwa mikwaju ya penati.

Azam FC ilianza kuifunga Yanga SC kwa penalti 5-3 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati, Kombe la Kagame Julai mjini Dar es Salaam.

Na Yanga SC ikalipa kisasi kwa ushindi wa penalti 8-7 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 katika mchezo wa Ngao ya Jamii Uwanja wa Taifa Agosti mwaka huu.

 

Niyonzima Hajawasili Kambini
FC Barcelona Kusaka Haki Yao CAS