Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula, ametoa onyo kwa wakuu wa Idara ya Ardhi kukaa na hati muda mrefu bila kuzipeleka ofisi ya kamishna msaidizi wa Aridhi kanda kukamilisha taratibu za utoaji.
Dkt, Mabula amesema kuwa “kuanzia sasa mkuu wa Idara ya Ardhi atakayekutwa amekaa na hati ya muda mrefu bila kuipeleka ofisi ya kamishna msaidizi wa ardhi kanda ataondolewa katika nafasi yake”
Ameyasema hayo alipozungumza na watendaji wa sekta ya Ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Miseyi mkoani Kagera akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya Ardhi.
Kauli hiyo ya Dkt Mabula, imefuatia baada ya kukuta baadhi ya hati katika halmashauri ya wilaya ya Misenyi zikiwa kwenye masijala ya Ardhi tangu mwaka 2017 bila kupelekwa ofisi ya Kamishna wa Ardhi Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kukamilishwa ili wahusika wapatiwe hati.
Na kuongeza kuwa baadhi ya halmashauri alizozitembelea wakati wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya Ardhi amebaini wakuu wengi wa idara wana hati kwenye ofisi zao kwa muda mrefu bila kufanya jitihada zozote za kuhakikisha hati hizo zinaenda ofisi ya Kamishna kwaajili ya kukamilishwa ili wahusika wapatiwe hati zao.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi, ucheleweshaji utoaji hati miliki za viwanja na mashamba siyo tu unawakera wananchi bali unaikosesha Serikali mapato ya kodi ya Ardhi kwakuwa wananchi wanakuwa hawajamilikishwa Ardhi kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyingine Dkt Mabula amewataka wananchi wa Miji ya Kyaka na Mtukula katika wilaya ya Misenyi mkoa wa Kagera kuchangamkia zoezi la urasimishaji makazi holela ambalo limeonekana kusuasua katika miji hiyo.
Akizungumza na wakazi wa Kyaka na Mtukula kwa nyakati tofauti Dkt Mabula amesema kuwa, haridhishwi kabisa na namna kasi ya urasimishaji inavyoendelea katika Miji hiyo ambapo takwimu zinaonesha wananchi waliojitokeza kwenye zoezi hilo ni wachache ukilinganisha na wakazi wa Miji.
Na kutolea mfano wa Mji wa Mtukula wenye kaya 842 zenye wakazi zaidi ya 3000 lakini ni watu 13 tu waliolipia fedha za kurasimishiwa maeneo yao na watu hao wamechangia jumla ya shilingi milioni moja na laki nane.
Aidha, amewataka wananchi wa Miji ya Kyaka na Mtukula kutofanya maendelezo katika eneo lolote ambalo hawajajua mipango yake ili kuepuka kubomolewa na kupoteza haki zao kwa kujenga katika maeneo yasiyo ruhusiwa ambapo ameitaka halmashauri ya wilaya ya Misenyi kupanga mpango wa matumizi bora ya Ardhi kwa lengo la kuwa na miji iliyopangika.