Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye jana alifanikiwa kutuliza vurugu iliyoibuka katika mdahalo wa kujadili hotuba ya rais John Magufuli aliyoitoa bungeni, ulioandaliwa na Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO).

Mdahalo huo uliofanyika jana majira ya jioni jijini Dar es Salaam uliingia dosari baada ya uongozi wa serikali ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) kupinga mdahalo huo wakidai kuwa hauendani na majukumu ya taasisi hiyo.

Walidai kuwa Taasisi hiyo imekuwa ikikaa kimya pale inapotakiwa kujadili masuala yanayowahusu wanafunzi huku wanafunzi wakiendelea kupata shida badala yake imekuwa rahisi kwao kuandaa mdahalo huo waliodai ni suala la kisiasa.

Rais wa DARUSO na viongozi wengine waliondolewa ukumbini hapo baada ya kupinga kwa sauti kuendelea kwa mdahalo huo kutokana na hoja hizo, suala lililopelekea kuamriwa kutoka nje ya ukumbi huo.

Hata hivyo, wakiwa nje ya ukumbi huo waliendela kupiga kelele, hali iliyomlazimu Nape aliyehudhuria mdahalo huo kuwafuata na kujadiliana nao.

Nape Na Wanafunzi

Baada ya kusikiliza maelezo yao ambayo yalikuwa yanarusha lawama kwa uongozi wa TAHLISO kushindwa kutatua kero zao, Nape aliwashauri wanafunzi hao kurudi ukumbini na kuendelea na mjadala na kwamba wawaondoe madarakani viongozi hao kwa kuwa ndio waliowachagua kwa kuwa wameshindwa kufanya kazi zao.

“Unajua tatizo lenu dogo, hawa viongozi mmewaweka wenyewe na kwa kawaida mwiba unapoingilia ndipo unapotokea. Hivyo, nyie ndio wakuwatoa, tumbueni majipu kama mnaona yapo,” alisema Nape.

Pia, Nape aliwaahidi wanafunzi hao kuwa atawasiliana na viongozi husika wa serikali kuhakikisha wanawashughulikia watendaji ambao wanachelewesha mikopo kwa wanafunzi na kushindwa kutekeleza majumu yao. Alitoa ahadi hiyo baada ya wanafunzi hao kumueleza kuwa takribani wanafunzi 89 wanatarajiwa kuacha masomo kutokana na kukosa mikopo huku TAHLISO na Bodi ya Mikopo wakishindwa kutoa majibu ya utatuzi.

“Naomba niwahakikishie kwamba ifikapo kesho (leo) wanaohusika tutakwenda kuwashughulikia ili wawajibike kwa sababu inaonekana kuwa tatizo maana wanafunzi wakigomba fedha zipo, wakikaa kimya hawapewi,” Nape aliwaambia wanafunzi hao.

Baada ya mazungumzo hayo, wanafunzi hao walikubaliana na Nape na kurejea ukumbini kuendelea na mdahalo.

Hodgson Amtaja Vardy Kabla Ya safari Ya Ufaransa
Kilichojili Baada Ya Madiwani Wa CCM Geita Kushindwa Kusoma Kiapo Kwa Kukosa Elimu