Rapa Nay wa Mitego ambaye mwezi jana Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) lilitangaza kumfungia kufanya muziki sambamba na kuufungia wimbo wake wa ‘Pale Kati’, ameibuka na kudai kuwa ameshamalizana na Baraza hilo.

Rapa huyo ameiambia Ayo TV kuwa amefanya marekebisho kama alivyoelekezwa na Baraza hilo na kwamba kuna ‘version’ nyingine ya wimbo huo ambazo mojawapo itaruhusiwa kuendelea kuchezwa kwenye media.

“In short, naweza kusema kuwa mimi na BASATA tumeshamalizana. Kuna vitu ambavyo walihitaji. Pale Kati ni wimbo ambao una version mbili, na kuanzia leo hii watu wanaruhusiwa kuendelea kurequest. Wimbo unaendelea kupigwa media zote,” alisema.

“Pale Kati imerudi kwenye media, na video mwezi ujao inaweza kuwa imetoka. Hatuna tatizo na BASATA ni walezi wetu tumemaliza hilo,” aliongeza.

Mbali na kuwa na version mbili za audio, alisema kuwa wimbo huo umefanyiwa video nne tofauti na kwamba zitaanza kutoka moja baada ya nyingine kuanzia mwezi ujao.

Nay alisema kuwa tayari video zimeshafanyiwa marekebisho kama ilivyokuwa imeelekezwa na BASATA hivyo zitaruhusiwa kuanza kuchezwa pindi zitakapotoka.

BASATA walitangaza kumfungia msanii huyo kwa sababu za kimaandili huku ikieleza kuwa licha ya kupewa onyo amekuwa akikaidi na kutoa nyimbo zisizokidhi vigezo. Baraza hilo limeshafungia nyimbo mbili za Nay ambazo ni ‘Shika Adabu Yako’ na ‘Pale Kati Patamu’.

 

Edgardo Bauza Akabidhiwa Mikoba Ya Gerardo Martino
Southampton Wasajili Mwingine Kutoka Ufaransa