Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT –Wazalendo Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema kwamba Zanzibar inahitaji kuingia katika Mageuzi yakayofanywa kwa kuzingatia Amani, ili nchi iendele kuendeshwa kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi wenyewe wanavyotaka.
Othman ambaye Pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo huko Chumbuni Wilaya ya Mjini Unguja alipozungunza katika Mkutano wa hadhara wa chama hicho akiwa katika mfululizo wa mikutano mbali mbali yenye dhamira ya kuelezea ahadi ya chama hicho kwa wananchi.
Amefahamisha kwamba hatua hiyo ni muhimu kwani itasaidia nchi iendeshwe kwa mujibu wa maono viongozi wa chama na wananchi wanavyotaka wenyewe ikiwa ni pamoja na kuzingatia haki ya kuchagua kiongozi na pia kuwa na uwezo wa kuwawajibisha na chama kiendelee kazi ya kuichunga na kuisimamia serikali.
Amesema kwamba hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kuendelea na kupiga hatua iwapo wananchi hawana uwezo na mamlaka ya kuwachagua na kuwawajibisha viongozi wao waliowachagua wanaoshindwa kuwajibika kulingana na mwatakwa ya wananchi kwa mujibu utaratibu.