Ndege ya Kenya Airways leo imelazimika kuahirisha kuruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) jijini Nairobi, baada ya mtu mmoja kudai kuwa kuna bomu kwenye ndege hiyo.
Polisi wameeleza kuwa mtu huyo aliibua suala hilo baada ya majibishano kati yake na mhudumu ya ndege hiyo, na baadaye akasikika akitamka neno ‘bomu’. Kauli hiyo ya abiria ilizua taharuki na woga ndani ya ndege hiyo na vyombo vya usalama vikajulishwa haraka.
Hata hivyo, baada ya upekuzi uliofanywa na kikosi cha kupambana na ugaidi, walibaini kuwa hakukuwa na tishio lolote ndani ya ndege hiyo. Kikosi hicho kinamshikilia mtu huyo kwa ajili ya kumhoji.
JKIA ulifungwa kwa muda kwa ajili ya kufanya upekuzi wa kina.
Shirika la ndege la Kenya Airways limetoa tamko lake na kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo majira ya saa saba mchana.
“Tishio la bomu limeripotiwa kwenye ndege yetu ya KQ 762, iliyokuwa inataka kuanza safari yake kutoka Nairobi kuelekea Uwanja wa Ndege wa OR-Tambo jijini Johannesburg,” Kenya Airways wameripoti.