Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amewataka Wanachama na Viongozi wa CCM Visiwani Zanzibar kuendeleza harakati za kuandaa mazingira rafiki ya kukipatia ushindi Chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
 
Ameyasema hayo Visiwani Zanzibar mara baada ya kuwasili visiwani humo kwa ajili ya ziara ya siku tatu ya kutembelea Mikoa miwili ya kichama ambayo ni Mkoa wa Kaskazini Unguja na Mkoa wa Kusini Unguja.
 
Amesema kuwa kila mwanachama anatakiwa kujipanga kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kubaki madarakani kwa ridhaa ya wananchi kwa ujumla, huku akiwasisitiza wanachama wa Mikoa ya Kaskazini Unguja na mkoa wa Kusini Unguja kuendeleza sifa na heshima ya maeneo yao yanayosifika kwa kuwa ngome imara za Chama Cha Mapinduzi.
 
Aidha, Ndugai amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kuimarika Kisiasa, Kiuchumi, Kidemokrasia na kimfumo huku baadhi ya vyama vya siasa vikiendelea kudhoofika kisera na kisiasa.
 
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Juma Mabodi amemhakikishia Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM kuwa hali ya kisiasa katika Mikoa anayoilea ipo shwari kutokana na historia nzuri ya maeneo hayo ambayo ndio yenye hazina kubwa ya mtaji wa kisiasa wa CCM.
 
Pia, amesema kuwa jukumu la ulezi wa Mikoa ni kubwa hivyo anaamini kuwa, Job Ndugai atafanya ziara yake hiyo ya kujitambulisha kwa wanachama pamoja na kuwapatia nasaha mbalimbali za kuwaongezea hamasa ya kuendelea kuwa wazalendo wa CCM na Taifa kwa ujumla.
 
Hata hivyo, katika ziara hiyo, Ndugai atatembelea maeneo mbalimbali na kuzungumza na wanachama kupitia vikao vya ndani sambamba na kukagua miradi iliyotekelezwa kupitia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Video: ACT ya Maalim Seif, Zitto kufutwa, Maswali magumu JPM mapato taifa
ACT- Wazalendo wapewa siku 14, 'Jielezeni kwanini chama chenu tusikifute?