Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile ameuelekeza uongozi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja.

Ndugulile ametoa agizo hilo katika mkutano wa 27 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa TPC ulilofanyika Dodoma ambapo amefafanua kuwa hivi sasa dunia ipo kiganjani na inatumia TEHAMA na kuitaka TPC kuongeza matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kuhudumia wateja ili kuongeza mapato ya Shirika na kuongeza gawio lake kwa Serikali.

“Sitarajii kuona TPC inaendeshwa kwa hasara, tumieni rasilimali za Shirika kwa ajili ya ustawi wa Shirika na sio ustawi wa mtu binafsi”, amesisitiza Ndugulile.

Aidha, ameipongeza TPC kwa utendaji kazi wao na ametaka mfanyakazi mmoja mmoja wa TPC kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kila kiongozi wa Shirika kusimamia vizuri eneo lake la kazi na kutekeleza majukumu yake.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa Baraza ni chombo muhimu sana maeneo ya kazi na lipo kisheria.

Naye Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Hassan Mwang’ombe amesema kuwa wajumbe wa Baraza hilo watakuwa na kikao cha siku tatu ambapo watajadili mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Shirika kwa mwaka 2021/2022,  matumizi ya mifumo mipya ya kidigitali kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za kila siku, sheria ya utumishi wa umma, wajibu na haki za kila mfanyakazi na kujadili maslahi ya wafanyakazi; mahusiano mahala pa kazi na nidhamu katika utendaji kazi.

Kaizer Chiefs wasubiri huruma ya CAF, RMFF
TFF yathibitisha kumtema Ndayiragije