Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji  Semistocles Kaijage amewataka wasimamizi wa Uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Jumapili hii kuhakikisha wanazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu ili kuepusha kubatilishwa kwa Uchaguzi.

Kaijage amesema hayo baada ya kupokea taarifa ya mwenendo wa Uchaguzi Mdogo wa Kata ya Kiwanja cha Ndege iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Morogoro Mjini.

Amesema kutozingatiwa kwa taratibu za Kisheria za Uchaguzi kunaweza kusababisha kubatirishwa kwa Uchaguzi mzima na hatimaye kusababisha Serikali kupata hasara kubwa, hivyo amemkumbusha Msimamizi wa Uchaguzi kuhakikisha wanafuata Sheria.

“Kwa kuwa miongozo yote mnayo ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Uchaguzi, hakikisheni mnatekeleza kila wajibu wa Kisheria katika zoezi hili kwa sababu kutozingatiwa kwa taratibu za Kisheria kunaweza kusababisha Uchaguzi ukabatilishwa” amesema Jaji  Kaijage.

Akitoa taarifa ya mwenendo wa Uchaguzi Mdogo wa Udiwani Kata ya Kiwanja cha Ndege,Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Morogoro Mjini, John Mgalula, amesema maandalizi ya Uchaguzi yana kwenda vizuri na wanakamilisha ujenzi wa baadhi ya vituo vya kupigia kura.

Hata hivyo, amesema kuwa kamati za maadili hadi sasa hazijapokea malalamiko yoyote na wanatarajia kukutana na wawakilishi wa vyama vya CHADEMA, CUF na CCM ili kuwakumbusha kuzingatia maadili ya Uchaguzi.

 

Baraka The Prince atamba, karibuni kuitwa baba
Mutungi afunguka kuhusu ruzuku ya CUF