Mbunge wa Viti maalumu wa chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe, Neema Mgaya amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi January 2016 hadi December 2018 ametumia pesa za kitanzania kiasi cha Milioni 144.5 katika kuunga mkono shughuli mbalimbali za maendeleo mkoani humo.
Ameyasema hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi zake kwenye baraza la umoja wa wanawake wa chama cha mapinduzi CCM (UWT) mkoani Njombe, ambapo amesema kuwa pesa hizo zimetumika kununua vifaa mbalimbali alivyo vitoa katika sekta tofauti mkoani humo ikiwa pamoja na Saruji, pamoja na mashuka kwaajili ya kuboresha huduma kwenye baadhi ya zahanati na vituo vya Afya mkoani humo.
Amesema kuwa amefanikiwa kutoa Vyereheni 370 katika vikundi vya akina mama vilivyopo kwenye Tarafa mbalimbali za wilaya zote nne za mkoa wa Njombe ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuelekea Tanzania ya Viwanda.
”Wajumbe mimi binti yenu kuanzia kipindi cha mwezi Januari 2016 hadi Disemba 2018 mwaka jana nimefanikiwa kutumia kiasi cha Milioni 144.5 pesa ambazo zimetoka kwenye mfuko wangu binafsi ambapo nimenunua vifaa mbalimbali ikiwemo Saruji, mashuka, pamoja na kutoa Vyerehani kwenye vikundi vya akina mama vilivyopo katika wilaya zote za mkoa wa Njombe,’’amesema Neema Mgaya
Aidha mbunge huyo ametoa vitabu vya masomo ya ziada kwa shule zote za Sekondari za serikali zilizopo mkoani Njombe pamoja na Shule mbili za sekondari zilizopo wilayani Ludewa ambazo zipo chini ya Idara ya Umoja wa wazazi wa Chama cha mapinduzi CCM mkoani humo.
Hatahivyo ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa viongozi wa chama cha mapinduzi CCM, Serikali pamoja na wananchi mkoani Njombe kwa lengo la kuchochea maendeleo jambo ambalo mh. Neema Mgaya amesema kuwa haliwezi kufanikiwa bila kuwa na umoja na mshikamano katika utendaji wa kazi.