Kiungo kutoka nchini Nigeria Nelson Esor Okwa kwa mara ya kwanza amefunguka, baada ya kuondoka kwa mkopo Simba SC na kutimkia Ihefu FC.

Kiungo huyo ambaye alisajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu huu akitokea Rivers United ya kwao Nigeria, amelazimika kuondoka klabuni hapo kwa mkopo baada ya kushindwa kufikiwa kiwango cha kuingia kwenye kikosi cha kwanza.

Okwa amesema yupo tayari kucheza Ihefu FC na ndio maana amekubali kujiunga nayo, huku akiamini anaweza kurejea Simba SC mwishoni mwa msimu huu akiwa na kiwango bora, kitakachomuwezesha kucheza kikosi cha kwanza.

Amesema kuhusu mazingira mapya aliyoyakuta Ihefu FC ni tofauti na Simba SC, lakini bado akasisitiza kupambana na kufanikisha mpango wa kurudi katika kiwango chake.

“Suala kubwa hapa ni kupambana katika klabu yangu mpya, nitahakikisha ninacheza kwa kiwango cha juu ili niweze kurudi Simba SC nikiwa vizuri na kuingia kwenye kikosi cha kwanza.”

“Mazingira hayawezi kufanana, lakini kilichonileta huku ni kucheza soka, kwa hiyo kazi kubwa iliyonileta Ihefu FC nitahakikisha naipambania ili kufanikisha kusudio la kurudisha kiwango changu.” amesema Nelson Okwa

Hadi anaondoka Simba SC kwa mkopo, Okwa alikuwa ameshacheza michezo mitatu ya Ligi Kuu pamoja na mchezo mmoja wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.

Tabasamu, tumaini jipya kwa wafugaji wa kisasa
Mwanahabari mmoja huuawa kila baada ya siku nne