Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema upimaji wa sampuli za wagonjwa waliokuwa wakiugua ugonjwa usiojulikana katika Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi umethibitisha uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mgunda ‘Leptospirosis Field Fever’.
Waziri Ummy ameyasema hayo hii leo Julai 18, 2022 wakati akiongea na waandishi wa Habari mara baada ya kuungana na timu ya Wataalam wa Afya waliokuwa wakifuatilia ugonjwa usiojulikana katika Wilaya ya Ruangwa Mkoa wa Lindi ambako kumezuka mlipuko wa ugonjwa huo.
Amesema, homa hiyo ya mgunda ni miongoni mwa magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na unasababishwa na bakteria aina ya Leptospira interrogans.
“Ugonjwa huu upo katika maeneo ya kitropiki yenye hali ya joto katika mabara ya Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kusini, Afrika, Asia na Australia, na Wanyama aina za Panya, Kindi, Mbweha, Kulungu, Swala, na wengine walioripotiwa kupata maambukizi haya na kuwa chanzo cha maambukizi kwa binadamu,” amesema Waziri huyo wa Afya.
Amesema, mtu anaweza kupata ugonjwa huo kwa kugusa mkojo au maji maji mengine ya mwili kutoka kwa wanyama wenye maambukizi, maji, udongo, au chakula kilichochafuliwa na mkojo wa wanyama wenye maambukizi au kunywa maji yaliyochafuliwa na vimelea vya bakteria wa ugonjwa huo huku maambukizi ya ugonjwa huu kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine hutokea kwa nadra.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Ummy amewataka wananchi kuchukua hatua zote stahiki za kujikinga na ugonjwa huo, ikiwemo kuepuka kugusa maji au vitu vilivyochafuliwa na mkojo wa wanyama na kunywa maji safi na salama ambayo yamechemshwa au kutibiwa.
Tahadhari nyingine zilizotolewa ni pamoja na kuwataka wagonjwa wenye dalili za homa, kuvuja damu, kichwa kuuma na mwili kuchoka kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili wapate matibabu sahihi.
“Wizara inaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na ugonjwa huu na kuendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa ugonjwa huu. Hivyo Serikali inawaasa Wananchi kutokuwa na hofu kwani ugonjwa huu unaendelea kudhibitiwa” amesema Waziri Ummy.
Ugonjwa wa Homa ya Mgunda, huambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kupitia uchafuzi wa mazingira ikiwemo vyanzo vya maji kutoka katika mkojo wa wanyama wenye maambukizi.