Kiungo kutoka nchini Rwanda Haruna Niyonzima amepongeza mifumo inayotumiwa na kocha mkuu wa Young Africans Luc Eymael, katika kipindi hiki ambacho bado wachezaji wanafanya mazoezi binafsi, kufuatia janga la maambukizi ya virusi vya Corona.
Niyonzima ambaye kwa sasa anafanya mazoezi ya Ufukweni, amesema kocha huyo ambaye kwa sasa yupo nchini kwao Ubelgiji, amekua akiwasilisha taarifa za namna wachezaji wake wanavyotakiwa kufanya katika kipindi hiki.
Amesema mifumo ya kocha huyo alietua nchini mwanzoni mwa mwaka huu akitokea Afrika Kusini alipokua akikinoa kikosi cha Black Leopards, imekua chachu ya wachezajai wengi wa Young Africans kuwa katika hali nzuri kiafya (FIT).
“Sisi tunajivunia zaidi mifumo mizuri ya kocha wetu na kwamba amekuwa akituhimiza mara kadhaa namna ya kujiweka sawa kabla ya ligi kurejea” alisema Niyonzima.
Mbali na kupongeza mifumo ya kocha Eymael, Niyonzima amesema ana hamu ya kuona ligi ikirejea ili aweze kupata nafasi ya kujumuika na wachezaji wengine wa Young Africans, kwa lengo la kurekebisha makosa ambayo yameiweka timu yao kwenye nafasi ya tatu, nyuma ya Azam FC na Simba SC wanaoongoza msimamo wa ligi.
“Hivyo kila mchezaji ana hamu ya kurejea uwanjani na kusawazisha mapungufu yote yaliyojitokeza kabla ya kusimama kwa ligi, naamini tutarejea na nguvu na kuchukua Kombe la Shirikisho au kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi” ameongeza Niyonzima.
Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa alama zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye alama 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa alama zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na alama 50 za mechi 28.
Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa alama zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC alama 22 mechi 28, Alliance FC alama 29, mechi 29, Mbeya City alama 30 mechi 29 na Ndanda FC alama 31 mechi 29.