Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa amewataka wamiliki wa viwanda nchini kuhakikisha wanakata bima za moto ili wapate fidia wanapokumbwa na majanga ya moto.

Bashungwa ametoa wito huo akiwa ziarani Karagwe mkoani Kagera jana, Mei 18, 2020 baada ya kutembelea na kukagua kiwanda cha kukoboa kahawa cha Amri Amir Al-HABSSY, kilichoungua kwa moto Mei 07, 2020.

Waziri aliona mashine zilivyoharibika baada ya kuunguzwa na moto ambao chanzo chake ni hitilafu ya umeme iliyotokana na radi kubwa iliyosababishwa na mvua iliyonyesha siku hiyo.

Akiongea baada ya kukagua, Bashungwa ametoa pole kwa mkurugenzi wa kiwanda hicho Karim Amri pamoja na wafanyakazi ambao kwasasa wamepoteza ajira zao, ambapo ameridhishwa na hatua ambazo zimekwishachukuliwa na wamiliki wa kiwanda hicho ambazo ni kufatilia bima kwaajili ya kulipwa fidia.

“Tunapokuwa na viwanda hatujui mambo ya kesho na keshokutwa, mambo ya ajari unaweza kupanga kila kitu lakini hakuna anayetegemea ajari itatokea muda gani, kwahiyo kupitia kiwanda hiki nitoe wito kwa viwanda vyote nchini tuwe tunakata bima, maana kiwanda hiki kimeungua lakini walikuwa na bima ya moto.”

Awali  meneja wa kiwanda hicho Daniel Ndayanse akitoa taarifa kwa Waziri alieleza  hasara walioipata baada ya kufanya tathimini ya hasara iliyotokana na kuungua kwa kiwanda hicho kuwa ni mashine za kiwanda ni takribani Tsh.1,328,940,000.00 na jengo la takribani Tsh. 49,275,750.00 na kuongeza kuwa kiwanda kilikuwa na waajiliwa wa kudumu 16 ambao wapo kwa kipindi chote cha mwaka na wakati wa msimu huwa kinaajili watu kuanzia 800 hadi 1000 kulingana na kazi ya siku.

Aidha, Meneja ameeleza kuwa “Kiwanda chetu tulikuwa tumekiimarisha kwa kukifanya cha kisasa ambapo tuliweza kuzalisha kati ya tani 50 hadi tani 65 za kahawa safi ambazo ni takribani gunia kati ya 800 hadi 1,000 kwa masaa 24, kwa kukoboa kahawa maganda kati ya tani 115 hadi tani 140 kwa masaa hayo 24 kama hakuna tatizo la umeme.”

Kwaupande wake mmiliki wa kiwanda amemshukuru Rais John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuimarisha na kuweka sera bora za viwanda kwa wawekezaji nchini.

Kufatia kukithiri kwa matukio ya moto wilayani Karagwe, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo ikiongozwa na mwenyekiti wake mkuu wa wilaya Godfrey Muheruka imeamua kujenga kituo cha zima moto na uokoaji ambacho kitakuwa kikisaidia kwenye ajali za moto pale zinapotokea.

Hata hivyo kitendo cha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya karagwe kuamua kujenga jengo la zima moto na uokoaji kikamshawishi waziri Bashungwa kuchangia mifuko 200 ya saruji na kuwataka wadau wa maendeleo kuchangia ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.

Niyonzima ampongeza Luc Eymael
Mazingiza: Ni mapema kutaja wanaoachwa