Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Filipe Jacinto Nyusi ameondoka nchini baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Rasilimali Watu (Africa Human Capital Heads of State Summit) uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 25 na 26 Julai, 2023.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam, Rais Nyusi amesindikizwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Faustine Kasike.
Katika Mkutano huo, Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi kujiuliza kama Bara walilolirithi kutoka kwa Waasisi waliotafuta Uhuru wa Afrika ndilo Bara wanalotaka kuwarithisha vizazi vijavyo au Wajukuu zao na kusema wakipata majibu watalijenga Bara la Afrika vizuri.
“Bara letu ni Bara lenye Watoto na Vijana wengi, habari hii ni nzuri na pia ni mbaya kwetu, hali hii inaweza kuwa nzuri na yenye tija tukiwekeza kwenye rasilimali Watu kwa kuhakikisha uwepo wa afya bora, elimu bora yenye stadi za maisha ili kujenga nguvu kazi yenye tija kama wenzetu wa Bara la Asia,” alisema.