Kiongozi wa chama cha muungano cha Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga amesema maandamano yaliyopangwa kufanyika nchini kote siku ya Jumatatu hayatafika Ikulu ya nchi hiyo, bali watatuma watawasilisha malalamiko yao kwa Rais Ruto.
Ameyasema hayo katika mahojiano na kituo cha habari cha Citizen, ambapo amesema kuwa muungano huo hautaandamana kinyume cha sheria hadi jumba la mlimani bali watatuma wawakilishi
Odinga amesema, kupitia kwa aliyekuwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya, muungano huo tayari umemwarifu Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome kuhusu maandamano hayo ya amani.
“Sisi ni watu wanaoheshimu na kujua sheria…Kiongozi wetu Wycliffe Oparanya alimwandikia Inspekta Jenerali wa Polisi kumfahamisha kwamba tutafanya mkutano. Wale ambao wataweza kufika Nairobi watakuja Nairobi na wasio na uwezo watafanya mikutano yao popote watakapokuwa,” amesema Odinga.
“Yatakuwa maandamano ya amani na wana risala ambayo wataipeleka katika afisi tofauti za serikali. Hapa Nairobi, tunazo pia memos ambazo tutaenda kumpelekea Rais. Akiwa Harambee House tutapeleka memo huko, akiwa Ikulu tutatuma watu wapeleke huko; sio umati. Tutatuma ujumbe kupitia watu wachache kupeleka ombi letu kwa Rais, sio umati mzima.”
“Tutatuma ujumbe kupitia watu wachache kupeleka ombi letu kwa Rais. Sijui kama nitakuwa sehemu ya timu lakini nikichaguliwa na wanachama wa chama, nitaenda.”
Aidha, alibainisha kuwa ikikataliwa kuingia, timu iliyochaguliwa itamwachia Mkuu wa Nchi ujumbe wao kwenye lango la Ikulu.
“Ikulu ni taasisi ya umma ambayo unaweza kwenda wakati wowote, sio ya kibinafsi. Sio kwamba ni eneo la hifadhi ambapo umma hauwezi kufika, ni afisi ya rais,” Odinga alisisitiza.
Alikariri akisema kwa vile serikali haikushughulikia masuala yao ndani ya muda wa siku 14 ambao walikuwa wametoa awali, maandamano hayo yataendelea hata baada ya Jumatatu hadi masuala hayo yatakapotatuliwa.
“Ikiwa (Ruto) angetaka kuzungumza, angefanya hivyo. Tulimpa siku 14 kurudi lakini hakufanya hivyo, alikataa na kutuhutubia kwenye televisheni tu. Naibu wake anazungumza kwa majigambo na anatumia lugha ya kudhalilisha,” amesema Odinga.
”Hii ndiyo lugha watakayoielewa. Maonyesho yataendelea zaidi ya Jumatatu hadi ulimwengu wote ujue kuna tatizo nchini Kenya.”