Shirika la matibabu ya wanyama la Uingereza lisilokuwa la kiserikali PDSA limemtuza medali ya dhahabu panya mkubwa, Magawa, kutoka Tanzania “kwa kujitolea kwake kuokoa maisha kupitia kazi yake ya kubaini mabomu hatari yaliyotegwa ardhini huko Cambodia”.
Panya huyo aliye na miaka saba alipewa mafunzo na shirika lisilo la kiserikali- Apopo kutoka Ubelgiji lenye makao yake nchini Tanzania.
Shirika hilo limekuwa likiwalea wanyama wanaofahamika kama – Panya Shujaa- kugundua uwepo wa mabomu ya kutegwa ardhini tangu miaka ya 1990.
Kwa wanyama 30 waliopewa tuzo hiyo, huyu ni panya wa kwanza na inadhaniwa huenda kuna hadi mabomu milioni sita ya kutegwa ardhini katika nchi hiyo ya kusini mashariki mwa bara Asia.
“Ni heshima kubwa kwetu kupokea tuzo hii, lakini pia ni ushindi mkubwa kwa watu wa Cambodia, na watu wengine duniani ambao wamekuwa wakiteseka kutokana na mabomu ya kutegwa ardhini,” amesema afisa mkuu mtendaji wa Apopo, Christophe Cox wakati shirika la habari la Press Association
Kulingana na Apopo, Magawa alizaliwa na kulelewa Tanzania akiwa na uzani wa kilo 1.2 na urefu wa senti mita 70, japo ni mkubwa kuliko spishi zingine za panya, Magawa ni mdogo ni mwepesi kiasi kwamba hawezi kulipua mabomu akitembea juu.
Magawa ana uwezo wa kusaka mabomu katika eneo lenye ukubwa wa uwanja wa mpira wa tennis kwa muda wa dakika 20 – jambo ambalo Apopo linasema itamchukua mtu aliye na kifaa cha kubaini vifaa vya chuma kati ya siku moja hadi nne.
Panya huyo anafanya kazi kwa saa moja na nusu kwa siku nyakati za asubuhi na anakaribia kustaafu, lakini mkurugenzi mkuu wa PDSA Jan McLoughlin amesema kazi yake katika shirika la Apopo ilikuwa ya kipekee na ya kuridhisha.
Kwa mujibu wa shirika lisilokuwa la kiserikali la kuondoa mabomu- HALO Trust, Cambodia imerekodi zaidi ya watu 64,000 waliojeruhuwa na wengine 25,000 kukatwa viungo vya mwili kutokana na mabomu ya kutegwa ardhini kutoka mwaka 1979.
Januari mwaka huu, Rais wa Marekani Donald Trump aliondoa vikwazo vya matumizi ya mabomu ya kutegwa ardhini kutoka Marekani ambavyo vilikuwa vimewekwa na Rais Barack Obama mwaka 2014.
Magawa ameweza kunusa mabomu 39 na silaha 28 ambazo hazijalipuka katika maisha yake.