Kiungo kutoka nchini Ufaransa, Paul Pogba amewataka wachezaji wenzake wa Man Utd kujiongeza wanapokua katika harakati za kusaka alama tatu muhimu za ligi kuu ya England, hususan wanapocheza kwenye uwanja wa Old Trafford.
Pogba ametoa wito huo kwa wachezaji wenzake baada ya Man Utd kuambulia matokeo ya sare ya bao moja kwa moja mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Wolverhampton Wanderers, kwenye uwanja wa Old Trafford.
Amesema inawapaswa kubadilika na kutambua umuhimu wa kucheza nyumbani, ambapo anaamini ndipo mahala sahihi pa kupata alama tatu, tofauti na inavyokua kwenye uwanja wa ugenini.
“Tunapokua nyumbani tunapaswa kucheza kwa kushambulia na kila mmoja ajitambue kama yupo nyumbani, haipendezi tunacheza nyumbani halafu tunajilinda, inakua kama tupo ugenini,” alisema Pogba baada ya matokeo ya sare dhidi ya Wolves.
“Tupo nyumbani, sioni sababu ya kuendelea kuuhusudu mfumo wa kuzuia kila wakati, ninaamini tukishambulia kila wakati kwenye lango la timu pinzani tutawaweka kwenye wakati mgumu na hatimaye tutapata bao/mabao, ambayo yatatuwezesha kupata alama tatu muhimu tukiwa kwenye uwanja wetu wa nyumbani,” alisema.
“Hatupaswi kufanya makosa ya namna hii katika michezo inayofuata, maana unapokua nyumbanhi thamani yako inatakia kuonekana kwa kupata ushindi, sasa itakua tunazuia kama tupo ugenini mpaka lini? Mimi sipendezwi na hili, tunapaswa kujiongeza kama wachezaji, tutumie uwezo wetu binafsi, endapo mbinu za kocha zinakua zimefeli.” Aliongeza Pobga.
Hata hivyo kauli hiyo ya Pogba inachukuliwa kama kupingana na mfumo wa meneja wao Jose Mourinho, ambaye mara nyingi hupenda kikosi chake kujilinda dhidi ya timu pinzani, pasi na kujali wanacheza ugenini ama nyumbani.
Mchezo dhidi ta Wolves unakua wa pili kwa Man Utd kuangusha alama kwenye uwanja wake wa nyumbani, baada ya kupoteza kwa kufungwa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Spurs majuma kadhaa yaliyopita.
Mwishoni mwa juma hili Man Utd watakua ugenini jijini London wakipambana na West Ham United kwenye uwanja wa London (London Stadium).