Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Pinda amewataka wadau wa msaada wa kisheria nchini kujenga na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na serikali ikiwa ni fursa ya kuweza kuwasilisha mapendekezo mbalimbali yenye tija serikalini kwa lengo la kuboresha zaidi sekta ya msaada wa kisheria nchini.
Kauli hiyo ameitoa jijini Dodoma wakati wa akifunga kongamano la siku mbili lililowakutanisha wadau wa sekta ya msaada wa kisheria takribani 120 kutoka Tanzania Bara na visiwani.
Lengo la kongamano hilo ni kutathimini utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa Kisheria ya Mwaka 2017 pamoja na kuangalia huduma ya msaada wa kisheria kwa ujumla.
Pinda, alisema kuwa serikali na wadau wa sekta ya msaada wa kisheria ni wadau muhimu katika utendaji kazi hasa katika sera, sheria, masuala mbalimbali ya haki ambayo yanawahusu wananchi.
“Ninaamini kwamba ili kuwepo matunda mazuri, kunahitajika uhusiano endelevu kati ya serikali na wadau wa sekta ya msaada wa kisheria. Kwa kutambua hilo, nawahakikishia kuwa ofisi yangu itakuwa wazi kufanya kazi na wadau wa sekta ya msaada wa kisheria kwa kupokea taarifa, ushauri na mazungumzo mengine muhimu kuhusu mambo mbalimbali yanayowakabili wananchi katika sekta hii nyeti nchini,” amesema Naibu Waziri Pinda