Spika wa Bunge mstaafu na mwanasiasa Mkongwe, Pius Msekwa amedaiwa kudanganya kuhusu historia yake na  Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyoiandika katika kitabu chake kinachoitwa ‘Uongozi na Utawala wa Mwalimu Julius Kambarage’.

Katika ukurasa wa 33 wa kitabu hicho, Msekwa ameeleza kuwa yeye ndiye kiongozi wa mwisho wa ngazi ya juu nchini kuzungumza na Mwalimu Nyerere kabla ya kifo chake, Oktoba 14 mwaka 1999.

Msekwa ameeleza kuwa alifika katika hospitali ya St. Thomas jijini London Oktoba 9 mwaka huo na alipata nafasi ya kuzungumza na Mwalimu kwa muda wa saa moja na nusu.

Hata hivyo, wasaidizi wa karibu wa Mwalimu Nyerere waliokuwa naye katika hospitali hiyo hadi umauti ulipomkuta walipinga ushuhuda wa Msekwa na kudai kuwa Mwalimu alikuwa amepoteza fahamu wiki mbili kabla ya kifo chake hivyo asingeweza kuongea.

“Sikiliza ndugu mwandishi, Mwalimu alikuwa kwenye comma (hakuwa na fahamu) kwa walau wiki mbili hivi kabla hajafariki. Tarehe 9 Oktoba ni chini ya wiki moja kabla ya kifo cha Mwalimu kilichotokea Oktoba 14 mwaka huo. Ni wazi hapo Msekwa hakusema kweli,”Msaidizi wa Mwalimu alimwambia mwandishi wa gazeti la Raia Mwema.

Msaidizi huyo alibainisha kuwa Rais Mstaafu William Mkapa ndiye kiongozi wa mwisho wa ngazi ya juu aliyezungumza na Mwalimu kabla hajapoteza fahamu.

Akijibu Madai hayo, Msekwa alisisitiza kuwa Oktoba 9 alizungumza na Mwalimu Nyerere na kwamba Mama Maria Nyerere alikuwepo.

Alisema kuwa baada ya kurejea nchini, alifikisha taarifa za hali ya Baba wa Taifa kwa aliyekuwa waziri Mkuu wakati huo, Frederick Sumaye.

“Nilipofika Dar es Salaam, moja kwa moja nilikwenda kwa aliyekuwa waziri Mkuu, Frederick Sumaye kumueleza hali ya Baba wa Taifa kama nilivyomwona. Nakumbuka nilimweleza kuwa hali yake inatia matumaini. Zilipokuja baadae habari kwamba Mwalimu ana hali mbaya, Sumaye aliniuliza mbona nilimwambia hali ni nzuri. Nikamwambia hali ilibadilika nilipoondoka, “alisema Msekwa.

Rais wa Colombia Ahalalisha Matumizi ya Bangi, ataja sababu
Sitta amfuata Dk. Slaa, apiga chini siasa