Jumla ya leseni 3,214 za madaraja C na E za madereva waliokuwa wakiendesha malori na mabasi ya abiria zimefutwa na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani nchini kutokana na madereva hao kukosa sifa ikiwemo wahusika kutosomea madaraja hayo.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Ng’anzi ambaye amesema leseni zilizofutwa ni kati ya leseni 20,940 zilizohakikiwa hadi kufikia Aprili 30, mwaka huu, (2023).

Amesema, leseni zilizofutwa zilionekana kutokidhi vigezo kwa sababu wahusika wamezipata visivyo halali na wameshushwa madaraja hadi ya awali ambayo ni D na B, na kwamba leseni 17,726 zilikidhi vigezo na tayari wamehakiki asilimia mbili ya leseni za madereva wa madaraja C na E.

Aidha, Kamanda Ng’azi ameongeza kuwa uhakiki awamu ya kwanza ulianza Machi Mosi kwa hiari kwa madereva kutakiwa kufika ofisi za wakuu wa usalama barabarani kuhakiki leseni zao na kazi hiyo ilipangwa kukamilika Aprili 30, mwaka huu.

Hata hivyo, amesema kwasasa wameongeza muda hadi Julai 31, 2023 ili kutoa nafasi kwa madereva kusomea madaraja E na C kwani kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu za jeshi, ni lazima dereva apite katika shule za udereva ili kumfanya kuwa na sifa stahiki za kumiliki leseni.

Chanzo: HabariLeo.

Azam FC yaahidiwa Mamilioni Nusu Fainali ASFC
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Mei 5, 2023