Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa Jeshi la Polisi visiwani Zanzibar limetosa ahadi yake kwake kuhusu kuandaa mkutano mkubwa wa hadhara.

Kauli hiyo ya Maalim Seif imekuja baada ya Jeshi la Polisi visiwani humo kuzuia kufanyika kwa mkutano wa hadhara wa chama hicho uliokuwa umepangwa katika kijiji cha Bubwini, mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo mkongwe, katazo hilo ni kinyume cha ahadi ya Jeshi hilo kwani lilimzuia kuendelea kufanya ziara zake katika ofisi na matawi mbalimbali ya chama hicho na kumtaka kuandika barua kuomba kufanya mkutano wa hadhara ili afikishe ujumbe wake.

“Nilipokuwa naenda katika ziara zangu za kichama, Jeshi la Polisi walinizuia nikiwa katika msafara na kunitaka niombe kibali cha kufanya mkutano wa hadhara. Mimi niliwajibu ‘hamtaniruhusu’, lakini wakashikilia niombe na ndipo nikaamua kuomba, lakini hatima yake wamekataa,” alisema Maalim Seif.

Alisema kuwa barua ya Jeshi la Polisi kuhusu zuio la mkutano huo imemueleza kuwa sababu ni kupisha mkutano mkubwa wa ibaya ya Waislamu inayofahamika kama Ijitimai itakayofanyika hivi karibuni katika Mkoa wa Kaskazini Unguja. Ibada hiyo itawakutanisha waumini wa dini hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mwanasiasa huyo ambaye mwaka jana alishiriki katika Uchaguzi Mkuu akigombea nafasi ya urais na kupinga kushiriki na matokeo ya uchaguzi wa marudio ulioitishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar,  alisema kuwa sababu hizo hazina mashiko kwakuwa chama chake kilipanga kufanya mkutano wake katika eneo la Kaskazini B na kwamba Ijimai itafanyika Kaskazini A. Alisema mikutano hiyo imepangwa tarehe tofauti.

CAF Yatoa Haki Za Matangazo Kwa Azam TV
ACT Wazalendo Kumpokea Zitto Kabwe Kimkakati, baada ya kulimwa adhabu Bungeni