Nguli wa masuala ya Uchumi nchini, Profesa Honest Ngowi amefariki dunia katika ajali ya gari mapema asubuhi ya leo Machi 28, 2022.

Habari zilizopatikana mapema leo zinasema Profesa Ngowi ambaye alikuwa ni Mchumi mbobezi akifanya kazi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro, amefariki yeye na dereva wake papo hapo, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuangukiwa na Kontena maeneo ya Mlandizi mkoani Pwani.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Pius Lutumo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza imetoka eneo la Mlandizi mkoani Pwani ikihusisha magari matatu.

“Ni kweli ajali imetokea leo saa 12 alfajiri ikihusisha magari matatu aina ya Noah, Land Cruiser alilokuwa anasafiria yeye na lori ambalo ndio chanzo cha ajali lilihama njia na kuiangukia Noah ubavuni kisha kuilalia gari ya Ngowi,” amesema Lutumo

Lutumo amesema hadi wanamtoa eneo la tukio alikuwa bado mzima akiwahishwa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi Mkoa wa Pwani.

Ofisa Habari wa Chuo cha Mzumbe, Rose Mdami amethibitisha kutoka kwa kifo cha Profesa Ngowi na kwamba Makamu Mkuu wa chuo hicho Profesa Lughano Kusiluka mekwenda katika Hospitali ya Tumbi Kibaha kwa ajili ya taratibu za utambuzi na kuanza maandalizi ya shughuli za mazishi.

Ndani ya siku tatu zilizopita Marehemu Profesa Ngowi alikua akitoa mafunzo ya ujasiriamali na uchumi kwa wanafunzi wachanga na waliomaliza vyuo vikuu wakisubiri ajira na amekuwa maarufu kwa kutoa mafunzo hayo akiwahimiza vijana kujiajiri.

Dembele amvuruga Rais Joan Laport
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Machi 28, 2022