Mojawapo ya kisa cha kustaajabisha kilichowaacha wapenzi wa mchezo wa soka mdomo wazi, ni tukio la mwaka 2015 nchini Mauritania.

Wakati wa mchezo maalum wa Super Cup, kati ya waliokuwa mabingwa wa ligi kuu nchini humo FC Tevragh- Zeina na waliokuwa washindi wa kombe la ligi klabu ya ACS Ksar, Rais wa Taifa hilo Mohamed Ould Abdel Aziz alihudhuria kwenye mchezo huo uliopigwa kwenye maadhimisho ya kumbukizi ya siku ya Uhuru wa Mauritania.

Jambo lililowastaajabisha wengi, ni kuwa katika dakika 63 Kipindi cha pili mwamuzi wa mtanange huo alipuliza kipyenga cha kumaliza mchezo huo timu hizo zikiwa sare ya kufungana 1-1.

Kwamujibu wa taarifa zilizotolewa, ni kuwa uamuzi wa kumaliza mchezo huo kabla ya kukamilika kwa dakika 90 ulitokana na agizo la Rais wa nchi hiyo aliyekuwa jukwaani akishuhudia mtanange huo ambao haukumfurahisha kutokana na kutokuwa na mabao mengi.

Taarifa za kuaminika zilizotolewa zinasema, Kiongozi huyo pia alikuwa ametingwa na majukumu mengi siku hiyo hivyo kuendelea kumsubiri mshindi kwenye mchezo huo kungempotezea muda zaidi.

Ikalazimu mikwaju ya penati iamue mshindi wa mchezo ili Rais aweze kushiriki zoezi la kutoa zawadi kabla ya kuondoka uwanjani hapo na kuwaacha mashabiki, wachezaji na viongozi wa timu zote mbili na bumbuwazi

Hata hivyo, Chama cha soka nchini Mauritania kilikanusha kuwa agizo la kumalizwa mchezo huo katika dakika ya 63 lilitoka kwa Rais wa nchi hiyo ili kuepuka adhabu ya kufungiwa na FIFA

Kwamujibu wa taratibu za FIFA, Serikali au mamlaka za kiutawala haziruhusiwi kuingilia kati shughuli za soka.

Lori lililouwa 13 Songea lilishindwa kupanda Mlima
Yafahamu Magonjwa ya Afya ya akili - Paraphilic disorders