Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo ameifuta rasmi Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma(CDA) na kuelekeza shughuli zote zilizokuwa zikifanyika hapo kuhamishiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.
Tukio hilo la kutia saini ya kuvunjwa kwa Mamlaka hiyo limefanyika mapema hii leo Ikulu Jijini Dar es salaam huku likishuhudiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Nyumba Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Paramagamba Kabudi.
Rais Dkt. Magufuli amesema kuwa ameamua kuivunja Mamlaka hiyo na kuhamishia huduma zake katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ili kuondoa mkanganyiko wa utoaji huduma kwa wananchi uliokuwa ukisababishwa na mgongano wa vyombo hivyo viwili, amesema kuwa kuendana na mahitaji ya sasa yamedhihirisha kuwa hakuna haja ya kuwa na CDA.
“Wananchi wa Dodoma wamelalamikia tatizo hili kwa muda mrefu sana, hata nilipokuwa katika kampeni zangu za uchaguzi za mwaka 2015 walilalamika sana, sasa nimetekeleza nilichowaahidi, naamini kwa utekelezaji huu malalamiko yatakuwa yamepungua, pia tutakuwa tumetatua kikwazo cha umiliki wa muda mfupi wa ardhi uliosababisha wawekezaji kushindwa kujenga viwanda Dodoma,”amesema Rais Dkt. Magufuli.
Hata hivyo, Rais Dkt. Magufuli ameagiza wafanyakazi wote waliokuwa wakifanya kazi katika Mamlaka hiyo wahamishiwe katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.