Serikali nchini, imedhamiria kuboresha maisha ya Watanzania hasa vijana kwa kuwawekea mazingira wezeshi ya kujiajiri kupitia shughuli za uvuvi na ukuzaji viumbe maji, ili kukuza kipato.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki wakati akizindua programu ya mafunzo atamizi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji kwa vijana iliyofanyika Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani.
Amesema Rais, Dkt. Samia amedhamiria kuwawezesha vijana kujiajiri na ndio maana katika mwaka huu wa fedha wa 2022/23 ameridhia kutengwa fedha kwa ajili ya vijana 500 watakaopatiwa mafunzo, ili waweze kujiajiri.
“tumepanga kuwawezesha vijana 500, awamu hii ya kwanza tumeanza na vijana 200 na watafuatia na vijana wengine 300, hii programu ni endelevu na mwakani tutaendelea kutenga bajeti,” amesema Waziri Ndaki.
Programu hiyo, inasimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, ikilenga kutimiza dhamira ya Serikali ya kuwaondoshea Vijana changamoto ya ajira.
Aidha, pia mafunzo hayo yatawaongeza mbinu za uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji, elimu ya ujasiriamali, kupata mitaji na mikopo ya taasisi za kifedha, kuanzisha na kusajili kampuni na elimu ya kutunza na kusimamia rasilimali fedha.