Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro amesema kuwa wamemkamata komando wa jeshi la Marekani akiwa anapeleleza katika mradi mkubwa zaidi wa mafuta.
Akihutubia mubashara kupitia televisheni ya taifa jana, Maduro amesema kuwa mtu huyo alikamatwa Alhamisi, Septemba 10, 2020 Kaskazini Magharibi mwa Jimbo la Falcon na alikuwa anapeleleza miradi ya Amuay na Cardon.
Maduro amemuelezea mtu huyo kuwa alikuwa komando wa Marekani aliyefanya kazi chini ya CIA nchini Iraq.
“Alikamatwa akiwa na silaha maalum, alikutwa na kiasi kikubwa cha fedha, kiasi kikubwa cha dola za Marekani na vitu vingine,” Aljazeera wamemkariri Rais Maduro.
Venezuela inakabiriwa na uhaba wa mafuta na iko katika harakati za kujaribu kujinusuru kupitia miradi mbalimbali ya mafuta, huku upande wa upinzani unaoungwa mkono na Marekani ikitumia hali hiyo kama fimbo kwa madai kuwa imetokana na usimamizi mbovu.
Hata hivyo, Serikali ya Marekani haijatoa tamko lolote dhidi ya madai ya Rais Maduro.
Taarifa hizo zimekuja mwezi mmoja baada ya Mahakama ya Venezuela kuwahukumu kifungo cha miaka 20 jela maafisa wa zamani wa jeshi la Marekani kwa kosa la kuhusika katika jaribio la kumpindua Maduro lililoshindwa, Mei 2020.