Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekutana na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Qatar, Muhamed Bin Ahmed Al-Kuwari na wadau kutoka sekta binafsi ya Viwanda na aliwakaribisha kuwekeza zanzibar kutokana na fursa zilizopo.
Dkt. Mwinyi amekutana na Wafanyabiashara hao baada ya kuwasili jana usiku jijini Doha, Qatar akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano mkubwa wa Jukwaa la Kimataifa la tatu la Uchumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa ZIPA Shariff Ali Shariff alieleza umuhimu wa kukutana kwa Mabaraza ya uwekezaji ya Zanzibar na Qatar ili kuimarisha uhusiano zaidi ambapo pia alielezea fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar zaidi kwa upande wa utalii kwani ujenzi wa hoteli kubwa za kifahari unahitajika kutokana na soko la utalii kuongezeka.
Aidha, fursa nyingine alizowakaribisha kuwekeza ni ukodishaji wa visiwa vidogo na pia aliwafahamisha kwa undani fursa zilizopo katika sera ya uchumi wa Buluu ambayo imewagusa zaidi wawekezaji hao hasa suala la uchimbaji wa gesi na mafuta na kuitangaza shamba la Makurunge Bagamoyo ambalo ni mali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar linalofaa kwa utalii na kilimo.