Maafande wa Polisi Tanzania wamesema hawatokubali kushuka daraja kinyonge, na badala yake watazing’ang’ania Simba SC na Azam FC kwa kushinda mechi hizo kujiweka katika nafasi ya kwenda kwenye hatua ya ‘Play Off’.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, John Tamba, amesema wanatambua presha walionayo mashabiki wa timu hiyo, lakini wamejiandaa vizuri kumalizika mechi mbili zilizobaki kwa ushindi ili kujiepusha kwenye janga la kushuka daraja.

“Tunaendelea na mazoezi yetu kwenye uwanja wa Chuo cha Polisi Moshi, tumejipanga vizuri kumalizia mechi zetu mbili, tunajua hatuko kwenye nafasi nzuri sana, lakini tukishinda mechi zetu mbili tunaweza kuepuka kushuka daraja, tunakwenda kucheza dhidi ya Simba SC na mwisho Azam FC, ni mechi ngumu na kubwa, lakini tumejiandaa kwa kila kitu na tunaendelea kuwaandaa wachezaji kimwili na kiakili kwa ajili ya kupambana,” amesema Kocha Tamba.

Kwa mujibu wa ratiba mpya, Polisi Tanzania itacheza dhidi ya Simba SC Juni 6 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi na pia itamalizia mechi zake msimu huu kwenye uwanja huo huo dhidi ya Azam FC, Juni 9.

Timu hiyo ipo kwenye hatari zaidi ya kushuka daraja kuliko timu nyingine yoyote baada ya Ruvu Shooting kutangulia.

Polisi inashika nafasi ya 15, ikiwa na alama 25, lakini ikisalia na mechi hizo ngumu na kama ikishinda itafikisha pointi 31, huku ikiombea timu za Mtibwa Sugar na KMC zipoteze mechi zao mbili kwani zote hizo zina alama 29.

Timu hizo mbili zikishinda mechi moja tu zitafikisha alama 32 na moja kwa moja itakuwa ni tiketi kwa Polisi Tanzania kushuka daraja.

Rais Mwinyi awakaribisha wawekezaji wa Qatar Zanzibar
Klopp azungumzia kinyonge EUROPA LEAGUE