Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametembelea ujenzi wa mradi wa hoteli ya kitalii ya nyota tano katika jiji la Mwanza, unaotekelezwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa moja ya jukumu lake la msingi ambalo ni uwekezaji.

Akitoa taarifa fupi ya mradi huo Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema kuwa ujenzi wa mradi huo ulianza mwishoni mwa mwaka 2013 na ulitarajiwa kukamilika mwaka 2016 lakini ulishindwa kukamilika kutokana na changamoto mbalimbali.

Rais, Samia Suluhu Hassan Akisikiliza maelezo ya mradi wa ujenzi wa Hoteli ya NSSF kutoka kwa Meneja Usimamizi wa Miradi Eng. Helmes Pantaleo mara baada ya kuwasili katika eneo la mradi huo Mkoani Mwanza.

Amesema, hivi sasa mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2024 kwa gharama ya shilingi bilioni 93 ambapo mpaka sasa mradi umetumia shilingi bilioni 57. Aidha, Mshomba amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo utafungua fursa mbalimbali za kiuchumi katika Mkoa wa Mwanza ikiwemo sekta ya Utalii.

Akieleza namna hoteli ya kitalii yenye hadhi ya nyota tano itakavyokuwa, Meneja Miradi wa NSSF, Mhandisi Helmes Pantaleo amesema kuwa Hoteli hiyo itakuwa yenye viwango vya kimataifa na itakuwa na huduma mbalimbali pindi itakapokamilika, huku Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Patrobas Katambi akitilia mkazo dhumani ya Mifumo ya Hifadhi ya Jamii Kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali.

Baada ya kutembelea na kupata maelezo juu ya ujenzi wa mradi huo wa hoteli ya Kitalii yenye hadhi ya nyota tano, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza NSSF kwa kuendelea kutekeleza mradi huo na kutoa wito kwa wafanyakazi wa NSSF kuendeleea kuchapa kazi na kutimiza lengo la NSSF la kulipa Mafao kupitia uwekezaji wanaofanya katika maeneo mbalimbali ikiwemo mradi huo wa hoteli.

Lionel Messi: Sidhani kama nitacheza 2026
Azam FC kufanya usajili wa kishondo 2023/24