Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein amewataka wananchi wa Zanzibar kufanya kazi na kutodanganyika kuwa ataondolewa madarakani na mtu yeyote.
Akizungumza jana visiwani humo mbele ya wananchi, Dk. Shein alieleza kuwa hakuna mtu au taasisi yoyote itakayotawala Zanzibar wakati yeye bado yuko madarakani.
“Hakuna atakayeweza kuingilia masuala ya Zanzibar, hakuna atakeyongoza Serikali hii wakati mimi bado ni ko madarakani. Msidanganywe,” alisema Dk. Shein.
“Hakuna cha Umoja wa Mataifa wala Katibu Mkuu gani atakayekuja kuiongoza Serikali hii wakati mimi niko madarakani,” alisisitiza.
Rais Shein ameyasema hayo wakati ambapo Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad amekuwa katika harakati anazoziita kuishtaki Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Umoja wa Mataifa akidai kupokonywa ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
CUF inashiriki uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Dimani, ikiwa ni miezi takribani tisa tangu chama hicho kisusie uchaguzi wa marudio uliofanyika mwaka jana baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25 akieleza kuwa ulikubwa na kasoro nyingi.