Mbali na kilichokuwa kikiendelea kwenye fainali za kombe la dunia nchini Urusi kati ya mwezi Juni 14 na Julai 15 mwaka huu, kivutio kingine kwenye mashindano hayo ni ushiriki wa Rais wa kwanza mwanamke wa Croatia, Kolinda Grabar-Kitarović. Google wamebainisha.
Kwa mujibu wa ripoti ya Google iliyowekwa wazi wiki hii, Rais Grabar-Kitarović ameongoza kwa kuwa mtu aliyetafutwa zaidi kwenye Google nchini Kenya mwezi Julai mwaka huu.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa Grabar-Kitarović kwa watumiaji wa mitandao nchini Kenya, alishika nafasi ya tatu kwa ujumla, akitanguliwa na mambo yaliyohusu Fainali za Kombe la Dunia pamoja na tukio la kupatwa kwa jua.
Wakenya walionesha kutafuta zaidi taarifa za fainali za kombe la dunia kuanzia hatua ya robo fainali lakini zaidi ni pambano la fainali kati ya Ufaransa na Croatia la Julai 15. Hivyo fainali hizo zilishika nafasi ya kwanza nchini Kenya kwa walio-Google.
Mwezi Julai, tukio la kupatwa kwa mwezi liliwavuta Wakenya wengi wakitafuta taarifa zake na kulifanya kushika nafasi ya pili kwa kutafutwa zaidi katika kipindi cha mwezi Julai kwenye rekodi za Google.
Kupatwa huko kwa mwezi kuliweka historia ya karne kwa kukaa muda mrefu zaidi ambao ni Saa moja na dakika arobaini na tatu.
Mtu mwingine aliyeweka rekodi ya kutafutwa sana na Wakenya akishika nafasi ya nne, ni mwanamke Ruth Kamande, mshindi wa taji la Miss Magereza akiwa mahabusu. Mrembo huyo alitafutwa zaidi na Wakenya kwenye Google baada ya mahakama kumhukumu kifo kwa kosa la kumuua kwa makusudi mpenzi wake kwa kumchoma visu mwaka 2015.