Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla ametoa wito kwa Wananchi kuhakikisha wanapokea Chanjo ya Corona kwa mustakabali wa Afya zao.
RC Makalla ametoa kauli hiyo akiwa ni miongoni mwa Viongozi waliopokea Chanjo hiyo wakati wa uzinduzi uliofanyika siku ya Jana ambapo amesema tangu amepokea Chanjo hiyo hajapata madhara yoyote ya kiafya.
Aidha RC Makalla amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha mfano kwa kuchanja na kutimiza wajibu wake wa kuwaletea wananchi Chanjo ili Waweze kuchanja kwa hiyari.
Pamoja na hayo RC Makalla ameendelea kuwasisitiza Wananchi kuchukuwa tahadhari dhidi ya Corona huku akisisitiza uvaaji wa Barakoa wawapo kwenye Vyombo vya usafiri na suala la Level seat.
Hayo yote yamejiri wakati wa ufunguzi wa Kikao Cha tathimini ya Lishe Mkoa wa Dar es salaam kilichohudhuriwa pia na Waziri wa Afya Mhe. Doroth Gwajima.
Akizungumza Katika kikao hicho RC Makalla amezielekeza Halmashauri zote za Mkoa huo kuhakikisha zinatenga fedha za kuwawezesha Maafisa Lishe kutekeleza majukumu yao.
Hata hivyo RC Makalla amewataka Maafisa Lishe kuhakikisha wanatoa Elimu ya kutosha kwa Wananchi kuhusu suala zima la Lishe ili kuepuka magonjwa mbalimbali ikiwemo Udumavu na utapiamlo.
Itakumbukwa kuwa Wakuu wa Mikoa yote nchini walisaini mikataba ya uboreshaji wa Lishe Katika maeneo yao kwa lengo la kuhakikisha jamii inakuwa na Afya Bora na Lishe Bora.