​Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Joackim Wangabo amewatahadharisha watumishi kutobweteka baada ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu, Zelote Stephen kustaafu na kumkabidhi kijiti cha utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya mkoa.

Amesema kuwa hatomwangusha Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumuamini na kumkabidhi madaraka hayo na kuahidi kuwa ataimarisha elimu inayoonekana bado ipo chini kwa ufaulu lakini pia kuendeleza kasi ya uzalishaji katika kilimo.

“Baada ya kusoma kabrasha hili la kukabidhiana ofisi kuna mambo mengi ya kuyazingatia ikiwemo, elimu, kilimo, ulinzi na usalama, utunzaji wa mazingira, uvuvi na uwekezaji katika viwanda. Hasa katika elimu maana mimba ni nyingi, kuna upungufu wa madawati, upungufu wa vyumba vya madarasa lakini pia kiwango cha ufaulu hakijafikia kile kilichopo katika ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo ni asilimia 80 kwa darasa la saba,”amesema Wangabo

Ameyasema hayo wakati wa  makabidhiano ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mapema leo hii tarehe 31/10/2017 katika ukumbi wa ofisi hiyo, jambo lililoshuhudiwa na watumishi wa sekretarieti ya Mkoa pamoja na baadha ya Halamashauri.

Hata hivyo, Kwa upande wake aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu, Zelote Stephen amewashukuru watumishi wote wa serikali katika Mkoa wa Rukwa pamoja na wananchi wa mkoa kwa kumpa ushirikiano katika kipindi chote alichokuwepo na kuwaomba waendeleze kumpa ushirikiano huo huo Mkuu wa Mkoa mpya ili naye aweze kufanya majukumu yake kwa ufanisi

TFF yashtukia njama za kumchafua Rais Karia
Mwamuzi Heri Sasii amtoa povu Haji Manara