Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo ametoa wito kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhusu kuharakisha ukarabati wa meli ya MV Liemba ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na wananchi wanaoishi katika mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Amesema kuwa wananchi hao wamekuwa wakiweka maisha yao hatarini kwa kutumia vyombo kama mitumbwi na boti ambavyo usalama wake ni mdogo ukilinganisha na meli kubwa ya MV Liemba ambayo usalama wake ni wa uhakika.
“Nitoe wito kwa Wizara, husika hii meli ya MV Liemba nimeambiwa hapa kwamba ikipita kwenda Zambia inaitwa ‘Our Baby’ mtoto wetu, sasa huyu mtoto wetu anaulizwa yuko wapi, Zambia wanauliza. Wizara husika twende haraka isimamie hili jambo, MV Liemba itengenezwe watu maisha yao yapo kwenye hatari kubwa ndani ya hili ziwa Tanganyika,” amesema Wangabo.
Ameyasema hayo alipotembelea mradi wa usanifu na ujenzi wa bandari ya Kabwe iliyopo kata ya Kabwe katika Wilaya ya Nkasi, ili kujionea maendeleo ya ujenzi huo ulioanza 1 Aprili, 2018 ambapo hadi sasa mradi huo umetekelezwa kwa asilimia 52 katika miezi 14 na unatarajiwa kukamilika, 1 Aprili 2020.
Aidha, mradi huo umegharimu Shil. Bil 7.49 ambazo ni fedha za Mamlaka ya Bandari nchini.