Wananchi waishio katika mwalo wa Malehe uliopo Kata Rubafu Halmashauri ya wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera wameiomba serikali kuwaongezea huduma ya vyoo ili kuweza kuepukana na msongamano wanaokumbana nao wakati wakupata huduma ya kujihifadhi.

Wametoa kero hiyo wakati wa mkutano wa kusikiliza kero za wananchi ulioandaliwa na ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo, ambapo wamesema kuwa kutokana na wakazi kuongezeka kila kukicha huduma ya choo inakuwa kero kutokana na kutokidhi mahitaji.

Wamesema kuwa kwasasa wana choo kimoja tu chenye matundu 6, matatu yakiwa ya wananume na matatu yakiwa ya wanawake kinashindwa kuhimili wingi wa watu huku kukiwa na mchanganyiko wa watu wazima na watoto suala ambalo linaweza kupelekea kutokea kwa magonjwa mbalimbali ya mlipuko.

”Katika Mwalo huu tupo wakazi wengi sana tena wengine wanakuja na kutoka, sisi kama wananchi tulitumia nguvu zetu kujenga choo hiki tunachokitumia na katika uzinduzi alikuja mwenyekiti wa halmashauri kukizindua, choo hiki sasa hakina uwezo wakutuhudumia sisi na familia zetu, tunaiomba serikali itujengee choo kingine ili kuepusha uchafuzi wa mazingira.” amesema mmoja wa wananchi.

Aidha, kero zilizoibuliwa na wananchi hao ni pamoja na kutopata huduma ya afya kwa masaa 24 kutoka katika kituo cha Zahanati Kyamalange, kuvamiwa na kupigwa na wanajeshi wa nchi ya Uganda kwa kile walichodai kutokujua mipaka ya Ziwani na kujikuta tayari wameingia kwenye maji ya nchi hiyo, kunyang’anywa mazao yao ya samaki na watu wanaosadikika kuwa ni askari polisi  pamoja na uhaba wa miundombinu katika shule yao ya msingi.

Akijibu kero hizo kwaniaba ya mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dkt.Themistocles Kamugisha amesema kuwa serikali kupitia halmashauri inampango wa kupanga makazi ya mwalo huo na kuwalasimisha na hapo ndipo watakapoweza kuwajengea choo kingine bora na imara mara baada ya kuachana na makazi holela yaliyoko pembezoni mwa ziwa.

Kuhusiana na kero ya kuvamiwa ziwani na wanajeshi wa Uganda Themistocles amesema kuwa kero hiyo ni kubwa hivyo ataifikisha kwa mkuu wa wilaya ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo amabaye anaweza kuja na kuwaonyesha wavuvi hao mipaka ndani ya ziwa hilo.

Kwa upande wake Afisa elimu wa wilaya ya Bukoba, Devotha Mtesigwa akizungumzia uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Kobukuza, amesema kuwa serikali inaleta zaidi ya shilingi milioni 300 katika halmashauri hiyo kwa elimu ya msingi fedha inayotumika kugharamia matumizi mbalimbali kwa shule zote za msingi.

“Serikali haianzishi boma au chumba cha darasa bali wananchi husika pale wanapoona watoto wao wanakosa chumba cha darasa wananwajibika kwa nguvu zao kuanza kujenga na baadaye serikali inakuja kuwasaidia kwa kuwaletea vifaa, nitoe rai kwa wazazi ambao wana watoto na watoto hao hawaendi shule kuwa serikali inatoa fedha ili watoto hao wasome sasa kama mzazi umeamua kukaa na mwano nyumbani tutakushughulikia kikamilifu.” amesema Devota

Mwalo wa Malehe ni miongoni mwa mialo mikubwa katika halmashauri ya wilaya Bukoba ambayo inakusanya mapato mengi ambapo licha ya kukusanya mapato hayo wananchi wa mwalo huo wanadai asilimi 20% ya mapato yao ambayo kwa miaka mitatu sasa hawajayapata huku mkusanyaji naye akidai asilimia 10% ambayo ni zaidi ya milioni moja.

Sudan: Mauaji ya wanafunzi yapelekea shule kufungwa nchi nzima
RC Wangabo ataka ukarabati wa Meli ya MV Liemba uharakishwe