Uongozi wa klabu ya Real Madrid, umeongeza juhudi katika suala la kumsajili mlinda mlango wa Man Utd, David De Gea kwa kutenga kiasi cha Pauni milioni 39 ambazo wanaamini zitatosha kumng’oa Old Trafford.

Real Madrid wamefanya maandalizi hayo huku wakijiwekea muda hasi Juni 15 wawe wamekamilisha dili hilo.

Kwa muda sasa uongozi wa klabu hiyo ya mjini Madrid, umekua ukimuwinda De Gea mwenye umri wa miaka 25, lakini walishindwa kutimiza azma hiyo kutokana na mkazo uliokua umewekwa na viongozi wa Man Utd.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya Man Utd zinaeleza kwamba, De Gea amekua akishinikiza kuondoka klabuni hapo, tangu alipoona hakuna muelekeo wa mashetani wekundu kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao.

Sababu nyingine inayotajwa kama kikwazo kitakachomuondoa mlinda mlango huyo, ni uwepo wa meneja Louis Van Gaal ambaye anaonekana kushindwa kutimiza ahadi ya kurejesha heshima kama ilivyokua chini ya utawala wa Sir Alex Ferguson.

Huenda De Gea akacheza mchezo wake wa mwisho akiwa na Man Utd mwishoni mwa juma hili, katika mchezo wa kuwania ubingwa wa kombe la FA ambapo mashetani hao wekundu watapambana na Crystal Palace.

Real Madrid wamekua hawana imani kubwa na mlinda mlango wao wa sasa Keylor Antonio Navas Gamboa, kama ilivyokua kwa Iker Casillas ambaye alitimkia FC Porto mwanzoni mwa msimu huu.

Lakini pamoja na kutokuwa na imani na mlinda mlango huyo kutoka Costa Rica, Keylor amedhihirisha ubora wake kwa msimu huu, ambapo alionekana kuwa imara langoni na kufikia hatua ya kuwa sehemu ya wachezaji waliosifiwa na mashabiki kwa kuifikisha Real Madrid kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ya nchini Hispania pamoja na kuwapeleka hatua ya fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.

TFF Bado Wanazongwa Na Jinamizi La Mabadiliko Ya Ratiba
NEW VIDO: ALICIOS ft. KIDUM - PETE (OFFICIAL 4k VIDEO)