Mabingwa wa Soka Barani Ulaya Real Madrid wamekamilisha Usajili wa Mshambuliaji Kinda kutoka nchini Brazil Endrick Felipe Moreira de Sousa akitokea klabu ya Palmeiras.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 16, anatajwa kuwa mwokozi wa taifa la Brazil kwa siku za usoni, kufuatia kuwa na kiwango bora cha kusakata Kabumbu na kufunga mabao.

Real Madrid imekamilisha usajili wa Kinda huyo, lakini rasmi atajiunga na klabu hiyo ya mjini Madrid mwezi July mwaka 2024.

Makubaliano hayo yamechagizwa na Kanuni za usajili za Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ ambazo haziruhusu Mchezaji chini ya miaka 18 kusajiliwa kwa makubaliano ya ajira tena ikiwa nje ya Taifa lake.

Hata hivyo Makubaliano ya Klabu za Palmeiras na Real Madrid yanatoa nafasi kwa Endrick kufanya ziara majuma kadhaa yajayo, katika klabu yake mpya ili kujonea mambo mbalimbali ya klabu hiyo, iliyopiga hatua kubwa kimaendeleo nchini Hispania na Barani Ulaya kwa ujumla.

Kwa furaha isiyo kifani Endrick ameiambia Tovuti ya Klabu ya Palmeiras: “Nitaishukuru klabu ya Palmeiras katika maisha yangu yote, Klabu hii itaendelea kuishi katika moyo wangu, leo nimebahatika kutimiza ndoto za kuwa sehemu ya wachezaji, watakaocheza nje ya Brazil miaka miwili ijayo, sitaisahau siku hii.”

“Mpaka ninakapojiunga rasmi na Real Madrid, ninaahidi kuendelea kutumika hapa kwa moyo wangu wote, na katu sitabweteka kwa mafanikio haya, ninaamini nitapambana zaidi ili kuiweka mahala salama klabu yangu ya Palmeiras.”

Naye Rais wa Klabu ya Palmeiras Leila Pereira amesema: “Tumekamilisha mpango mkubwa wa makubaliano kati yetu na Real Madrid, ni faraja kwetu kuona kijana Endrick anapiga hatua kutoka hapa kwetu.”

“Ukitazama Mpango kazi wa Real Madrid kuhusu kumuendeleza kijana huyu, utaamini ana safari kubwa ya matumaini ambayo binafsi naamini ataifikia, na kuwa mchezaji mkubwa duniani kwa miaka ijayo.”

Endrick tayari amehaingia katika vitabu vya kumbukumbu vya klabu ya Palmeiras kwa kuweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo aliyefunga mabao mengi.

Pia Kinda huyo amekua sehemu ya wachezaji chini ya umri wa miaka 17 wa Brazil waliofunga mabao matatu katika michezo saba ya Ligi Kuu ya nchini humo ‘Serie A’ msimu huu.

Lionel Messi: Alvares ametufikisha hapa
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Desemba 16, 2022