Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete amekana kuhusika kwa namna yoyote katika sakata la tuhuma za ufisadi wa mabilioni unaodaiwa kufanywa kupitia kampuni ya Lugumi iliyopewa tenda ya kusambaza mashine za kutambua alama za vidole kwenye vituo vya Jeshi la Polisi.

Taarifa zilizotolewa na gazeti moja la kila siku zilieleza kuwa Ridhiwani ni mmoja kati ya wamiliki wa Kampuni ya Lugumi, ambayo wamiliki wengine waliotajwa na gazeti hilo ni Said Lugumi pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema.

Taarifa za ripoti ya ukaguzi ya Mwaka wa Fedha 2013/14 ya mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zilizowasilishwa mbele ya Kamati ya Kudumu Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilionesha kuwa Kampuni ya Lugumi ilipewa tenda ya kusambaza mashine hizo katika vituo 108 vya polisi nchini, lakini licha kusambaza mashine hizo kwenye vituo 14 tu, tayari imeshalipwa asilimia 99 ya fedha zote. Mkataba huo ulikuwa na thamani ya shilingi billion 37.

PAC ambayo iko chini ya Uenyekiti wa Aeshi Hilaly ilitoa siku 7 kwa Jeshi la Polisi kuwasilisha nyaraka za mkataba walioingia kati yake na Kampuni hiyo ya Lugumi.

Akijibu tuhuma za kumhusisha na Kampuni hiyo, Ridhiwani alisema kuwa taarifa hizo ni za uzushi na kwamba yeye na Said Lugumi wanafahamiana kawaida kama marafiki na hana uhusiano na kampuni hilo.

“Mimi si mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo, hilo ni jambo la msingi kabisa watu waelewe na sijawahi kufanya biashara yoyote na Lugumi. Said Lugumi ambaye ni mmiliki wa kampuni hiyo tunafahamiana naye na ni rafiki yangu,” alisema Ridhiwani.

Azam FC Kuwakosa Kapombe, Sure Boy
Tanzia: Ndada Kosovo afariki